Mahubiri

Hotuba kwa ajili ya miaka  25 tangu kuanzishwa kwa Misioni ya Masista Wa-Ursula wa Tanzania: Mkiwa, 25 Septemba 2015

 

Namshukuru Baba Askofu Mapunda kwa heshima aliyonipa kwa kunialika kuwa mtoa hotuba katika tukio hili kubwa na muhimu ambalo tunaliadhimisha: miaka 25 ya kuwepo masista ya mt. Ursula hapa Mkiwa, na Tanzania kwa jumla.

Nashukuru pia masista ambao walikubaliana na mwaliko wa Mhe. Baba Askofu. Nawasalimu viongozi wote waliopo, hasa kwa upande wa Shirika la Masista wa Mt. Ursula na waalikwa wote na wenyeji wote ambao kwa  moyo wa ukarimu sana walinikaribisha.

Wakati ambapo nilijiandaa kutoa hotuba hii nilianza kutafakari, je, niseme nini katika adhimisho kama hii, ambapo wengi kwa wakati mbali mbali watatoa hotuba zao na watapongeza masista na kuwashukuru kwa uwepo wao na kwa kazi nyingi na muhimu za huruma ambazo tangu mwanzo walianza kuzifanya kwa ajili ya Kanisa na hasa kwa ajili ya watu wengi waliopata na wanaoendelea kupa huduma zao.

Kawaida wakati ambapo tunafanya sherehe kama hii, moja kwa moja tunaanza kutaja faida kubwa washerekewa walizoleta kwa watu wa mahali walipokwenda, kwa mfano kwa ajili ya Jimbo, kwa ajili ya watu wa hapa Mkiwa kwenywe na hatimaye kwa ajili ya mahali pengine pote waliposambaza huduma yao. Bila shaka kufanya hivyo ni vizuri, lakini hakutoshi. Kwa kufanya hivyo tu hatuingii katika kiini cha sherehe yenyewe. Masista wanasherekea siku hii siyo tu kwa kutuonesha mambo makubwa waliofanya, na bila shaka walifanya mambo makubwa, lakini hasa kwa kutushirikisha sisi sote katika shukrani wanayotaka kutoa kwa Mungu aliyewazesha kufanya hayo yote na kutushukuru hata sisi ambao tulikubali huduma yao na tuliwaamini kwamba wanaweza kutoa huduma nzuri.

Ili kuelewa vizuri maana ya sikukuu tunayosherekea nilienda kwanza kusoma masomo ya Misa tulioyoyasikia kusomwa sasa hivi. Kama tulivyosikia katika masomo haya matakatifu, nimeelewa kwamba masista walichagua masomo yanayoeleza shukrani za watu kwa Mungu kwa kuwa aliwajalia watu wake neema na baraka zake. Waisraeli wanasimulia fadhili za Mungu kwa sababu aliwafanya kuwa watu wake na kuwaneemesha kwa kuwapatia mahali walipoweza kujijengea kama taifa. Paulo, naye, katika somo la pili tulilosikia anamshukuru Mungu si tu kwa neema aliyopata yeye kutoka kwake Mungu, bali kwa neema ambayo kwa njia yake Paulo wakristu wa Korintho waliipata kutoka kwa Mungu. Kwa njia ya neema hii Wakorintho walipata kumjua Mungu na wakawa jumuiya moja. Paulo anatumia neno moja ambalo ni muhimu kulikazia, neno uaminifu, kwamba Mungu alikuwa na ni mwaminifu. Katika somo la injili tulisikia masimulizi ya muujiza wa Yesu wa kuwaponya watu kumi wenye ukoma. Kati yao aliyeona umuhimu wa kurudi nyuma na kumshukuru Yesu kwa kuponyeshwa ni mmoja tu, naye ni mgeni asiyetambulikana kama mtu wa taifa teule la Mungu.

Nilijiuliza: kwa nini masista walichagua masomo haya? Kwa upande mmoja sikuona gumu jibu nililojitoa. Masista kwa adhimisho hili wanatambua kwamba Mungu aliwajalia neema nyingi na fadhili na kama wateuliwa wakamilifu wanataka  kumshukuru Mungu. Ni jambo la maana kabisa, ambalo linatakiwa kufanyika kwa kila mmoja ambaye anatambua kwamba bila wito kutoka kwake Mungu na msaada wake hawezi kitu.

Lakini nilipokwenda ndani zaidi kuchambua masomo haya matakatifu niliona kwamba sababu haikuweza kuwa hiyo tu. Ingekuwa sababu rahisi mno, ijapokuwa muhimu na ya lazima. Nilibuni kwamba masista walikuwa na sababu nyingine. Na nikaanza kujiuliza: masista wanamshukuru Mungu na kwa kumshukuru Mungu wanatushukuru hata sisi kwa sababu gani?

Kwa sababu walianzisha shirika hapa Tanzania na shirika kukua kwa kasi kubwa? Kwa sababu walipata watu wema ambao waliwasaidia kwa hali na mali ili kulikuza shirika? Kwa sababu ya afya nzuri ambayo walipata waanzilishi wa shirika ilyowawezesha kulisindikiza shirika kwa muda huu wote? Kwa sababu walipata masista wengi watanzania ambao wanaendesha taasisi walizoziweka kwa ujuzi na utalamu? Bila shaka hizi ni sababu zote za kumshukuru Mungu. Lakini kweli, je, sababu ni hizi tu?

Nikarudia masomo matakatifu waliyochagua na kutushirikisha katika ibada hii ya Misa na nikaona kwamba kuna neno moja ambalo katika somo la pili linaweza kutoa mwanga zaidi katika kuelewa umuhimu wa adhimisho hili tunalosherekea. Nalo neno ni hili: Mungu ni mwaminifu.

Mimi naijua kidogo historia ya masista walipokuja Tanzania na hasa Mkiwa. Najua kwamba mimi mwenyewe niliwaalika wafikirie kujiweka Mkiwa. Kwa kweli Mkiwa hapakuwa mahali ambapo kulikuwa hakuna wakristu. Huku Mkiwa ilikwepo tayari jumuiya hai ya wakristu, kanisa la kigango tayari limekuwa limejengwa, zilikwepo jumuiya ndogo ndogo, lilikwepo kundi la vijana wakatoliki, halmashauri ya Kanisa, na mambo mengine mengi ambayo yanaonesha uhai wa Kanisa la mahali. Kwa kuja Mkiwa masista walileta nini katika jumuiya wa wakristu wa Mkiwa, na sio Mkiwa tu, lakini hata katika Kanisa la Parokia ya Itigi, na katika Jimbo, na Kanisa la Tanzania kwa jumla?

Bila shaka hawakuleta ukristu, ambao nilivyosema tayari ulikwepo, ijapokuwa inawezekana kwamba wengine kwa njia yao walipata ubatizo. Kama hawakuleta ukristu, je masista walileta nini? Ni dispensari waliyoleta, au shule ya watoto wadogo, au shamba la kilimo, au shule le homekraft kwa wasichana, au huduma kwa yatima na wasiojiweza? Bila shaka mambo hayo yaliletwa na wao, lakini je, kweli, ni hayo ambayo kwa ajili yao waluikuja masista Mkiwa na Tanzania kwa ujumla?

Turudie lile neno ambalo tulisikia katika somo la pili, ambalo linasema kuwa Mungu ni mwaninifu. Sasa uaminifu wa Mungu kwa watu wake na taifa lake unaonekana namna gani? Ni kwa njia gani tunaweza kuona kwamba Mungu ni mwaminifu, na ni mwaminifu katika kitu gani?

Mungu ni mwaminifu katika kumjalia kila moja, na kila jumuyia na kila Kanisa wingi wa karama zake. Masista walipokuja Mkiwa hawakuleta ukristu nilivyosema, lakini walileta kitu ambacho hakikwepo bado, yaani karama ya shirika lao. Kwa kuelewa vizuri neno hili lazima tujikumbushe sehemu nyingine ya waraka huu wa Paulo kwa wakristu wa Korintho: sura ya 12 anapowaelezea wale wakristu wa zamani kwamba Mungu alimjalia kila mmoja wao karama au vipaji ambavyo ni vya kwake tu na anatakiwa kuvikuza na kuvishirikisha kwa wenzake ili kujenga jumuiya imara. Na jumuiya imara ni wakati ambapo watu wanajengana na kukamilishana pamoja wao kwa wao kwa kushirikishana vipaji kwa ajili ya Mungu. Jambo ambalo lipo kwa kila mmoja binafsi, lipo pia kwa kundi la watu au kwa mashirika ya kidini. Mtu binafsi anajaliwa na Mungu kipaji chake, pengine ni uwezo wa kuelewa, pengine ni nguvu ya kufanya kazi, pengine ni uvumilivu wa kuvumilia mateso, pengine ni uwezo wa kuongoza, pengine ni uwezo wa kushauri watu, au wa kuponya, na vipaji vingine vingi sana. Tunatambua kwamba kila kipaji hiki ni zawadi yake Mungu kwa kila mmoja. Na Paulo anatukumbusha kwamba lazima tushirikishe kipaji au vipaji vyetu binafsi kwa wengine ili kujenga jumuiya imara kamilifu ya wakristu.

Mungu anatoa vipaji vyake sio kwa ajili ya mtu mmoja tu, bali pia kwa ajili ya kundi la watu. Au niseme vizuri zaidi. Anatoa kwa mtu mmoja ambaye lakini ana uwezo wa kuwavutia wengine kuungana naye kukuza na kusambaza vipaji hivi. Mungu alimjalia Mt. Ursula Ledochowska vipaji ambavyo kwavyo aliwavutia wengine kwa kuwa alikuwa tayari aliwahirikishia wengine. Mtasikia zaidi kuhusu mwanzilishi huyu wa shirika la Masista wa Moyo Mtukufu wa Yesu. Mimi sio mtaalam. Ninachojua ni kwamba kipaji chake kilikuwa ni ibada kubwa kwa Yesu na moyo wake  na mwelekeo wake (utume wake) ulikuwa ni elimu na malezi kwa watoto na vijana. Ursula aliona katika moyo wa Yesu alama ya ule upendo ambao ni msingi wa uhusiano wake Mungu nasi na wetu kwake Mungu. Mtakatifu huyo aliweza kuwavutia wengine waliotambua moyoni mwao upendo kamilifu wa moyo wa Yesu kwao, wakajenga jumuiya ambayo ikawa Shirika: Shirika la masista wa Moyo Mtukufu wa Yesu mteswa. Nieleze wazo hili kwa kutumia maneno yenye wa Mt. huyu: Ninyi ni sehemu ya ufalme wa moyo wa Yesu, tafuteni kwa hiyo kitu kimoja tu: kupanua huo ufalme, huo utawala wa moyo  wa Yesu katika mioyo na msiangaike na kitu kingine. Moyo wa Yesu anawapa chochote kile ambacho mnahitaji kwa ajili ya wokovu wenu.

Kwa kuja Tanzania, na hasa katika Kanisa la jimbo la Singida na kigango cha Mkiwa, masista ambao nilivyosema hawakutuletea ukristu, walituletea karama au kipaji hiki: idaba kwa moyo mtakatifu wa Yesu. Siku hizi watalamu wanasema Tasaufi, lakini mimi naogopa kutumia hili neno, hasa kwa sababu silielewi vizuri, kwa hiyo natumia neno nililozoea kulitumia, yaani ibada kwa moyo wa Yesu. Ibada hii ni zawadi ambayo Mungu kwa kupitia masista hawa anatufanyia kila mmoja wetu, na kanisa la Singida na kanisa la Tanzania. Ni mpango wake Mungu, wala sio bahati, bali narudia kusema, ni mpango wake Mungu kwamba masista walifika hapa ili tuongeze katika Kanisa letu kipaji hiki. Nasi tuonyeshe uhai wa kipaji hiki kwa kuwa karibu nao masista hawa, kushirikiana pamoja maisha, kusali pamoja nao na kushiriki nao kwa kazi wanazozifanya kwa ajili hasa ya elimu na malezi ya vijana na watu wasiojiweza.

Masista mpaka sasa wanaongozwa na mawazo na mawaida ya mwanzilishi wao. Mengi huyu manzilishi alisema na kuyafanya ambayo hata mimi siyafahamu vizuri. Lakini kuna mengine ambayo napenda kushirikiana nanyi, kwa sababu kweli adhimisho hili lisipite bila kuwa na kumbukumbu nzuri ya kulisha roho zetu. Mama Ursula aliwaachia wosia masista wake kabla ya kufa kwake, akiwa mzee wa kutojiweza tena. Wosia hizi ni nzuri na zinaongoza maisha ya masista hadi sasa. Ningependa kuwasomea zingine. Nilivyosema hizi ni karama za Mungu kwa ajili yetu Mtakatifu huyu na masista wafuasi wake walizotuletea, ambazo bila masista kuwepo hapa kati yetu tusingeweza kuzipata au tungezipata kwa namna tofauti.

Tusikilize anachosema Mt.Usrula. Kumbukeni mambo mawili: uwema unafahamu daima kushukuru kwa ukunjufu hata kwa mambo madogo madogo; uwema unafahamu kupokea na kukubali misaada midogo midogo ya kitu chochote kila mmoja anachofanyiwa. Ishini daima katika amani na upendo kwa wote. Waacheni wengine huru ili wawe na amani. Muweni wema zaidi, muweni wenye kujaa sadaka na utayari kama Yesu kwa kuyatoa maisha yenu kwa ajili ya wengine.

Au maneno haya mengine: Mpende Yesu, mpende juu msalabani, mpende kwenye tabernakulo, mpende katika mapenzi ya Mungu na daima mtakuwa wenye furaha, na hii furaha itawageuza kuwa jua kwa ajili ya wengine. Hii sio kazi ya ajabu? Kumbuka kwamba mtu mwenye furaha yeye mwenyewe ni mtume ambaye bila kufahamu anainjilisha na kuwapeleka watu  kwa Mungu, kwa sababu anaeleza kwa wanadamu bila kutumia maneno bali kwa tabasamu.

Na ningependa lumaliza kwa sala hii ya Mt. Ursula:
Ee Bwana unijalie kuwa mionzi ya jua,
inayoeneza mahali popote faraja na furaha,
inayowatangazia watu wote utukufu wako na upendo,
pia kama ni tabasamu lako,
ee Mungu wa milele.

Mengi sana zaidi Mt. Ursula alisema na alifanya ambayo masista bila shaka wanayafahamu vizuri na wanajaribu kuyaiga ili karama yake iweze kuendelea kwa manufaa yako na ya Kanisa la Tanzania. Ila mimi nione nimalize hapa.

Namaliza lakini kwa kurudia masomo ya shukrani tuliyoyasoma. Shukrani inatufaa sisi: shukrani kwa masista waliouitikia wito wa Mungu wa kuja katika kigango, parokia na jimbo letu na kutuletea karama na vipaji vyao. Bila wao kuja sisi tusingekuwa na kipaji hiki, au tungekuwa nacho kwa namna tofauti. Kwa maisha yao ya ukarimu, uvumilivu, wastani, ukimya walituonyesha kwamba Mungu ana moyo mkubwa, wa kutupenda wote na kutufanya kuwa watu wa taifa lake.

Na hasa tunamshukuru Mungu ambaye alitutazama kwa moyo wa upendo, au upendeleo kwa kututumia masista hawa ambao kwa kazi yao na mifano ya maisha yao ya sadaka, utaratibu na ujasiri walituvutia kuingia katika familia hiyo kubwa ya Yesu, familia ambapo inajaa upendo na mshikamano kati ya watu  wote.